- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mafunzo haya yametolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Raisi-TAMISEMI kupitia programu ya Shule Bora katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
Mafunzo yalitolewa kwa awamu mbili ambapo awamu ya Kwanza ilifanyika tarehe 31 Julai 2023 ikiwahusisha Viongozi wa elimu ambao ni Afisa Taaluma wa Mkoa, Waratibu wa Program ya Shule Bora kutoka kila ofisi ya Afisa Elimu Wilaya, Wakuu wa Shule Ishirini na tano (25) na Maafisa Elimu Kata (10).
Katika hotuba ya Ufunguzi, Afisa Elimu wa Mkoa Dr. Elpidius Baganda aliwasisitiza viongozi kuzingatia mafunzo kwani yanahusu utekelezaji wa Elimu jumuishi ambao ni msingi wa utoaji wa elimu kwa wote bila ubaguzi. Aidha, Dr Baganda alisisitiza kwamba mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo viongozi kwa kufahamu mbinu bora za kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wa makundi yote kwa kuzingatia mahitaji yao.
‘’…Viongozi mlioko hapa hakikisheni mafunzo haya yanafanyika katika jumuiya za Ujifunzaji (JzK) katika kila shule na hivyo kuwafikia walimu wote wa Mkoa wa Singida’’ Alisisitiza Dr Baganda.
Awamu ya pili ya mafunzo ilifanyika tarehe 01 hadi tarehe 04 Agosti, 2023 ikiwahusisha walimu Hamsini (50) ambao ni wawezeshaji rika na walimu wa KKK kutoka shule za Msingi ishirini na tano (25) ndani ya Mkoa wa Singida.
Akizungumza katika mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa Bi. Regina Yaghambe ambaye ni Afisa Taaluma Mkoa wa Singida alisema kuwa mafunzo haya yatawajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu jumuishi za ufundishaji na ujifunzaji ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wa makundi kumi na tatu (13) kama yalivyoainishwa katika Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2021/22 hadi 2025/26.
‘’…Ni Dhahiri kwamba madarasa yetu yana wanafunzi wenye mahitaji tofauti ya ujifunzaji, hivyo mafunzo haya ni fursa muhimu kwa kila mwalimu kupata mbinu za uboreshaji wa mazingira rafiki na fikivu kwa ujifunzaji,upimaji endelevu kulingana na mahitaji ya mwanafunzi, uandaaji na utumiaji wa mpango binafsi wa ujifunzaji wa mwanafunzi kulingana na mahitaji maalumu aliyonayo na mbinu za ujifunzaji kwa wote.’. Alisisitiza Bi Regina.
HALMASHAURI YA WILAYA MANYONI
Sanduku la Posta: S.L.P 60 MANYONI
Simu: +255 26 2540136
Namba ya Simu: +255 26 2540136
Barua Pepe za Watumishi: ded.manyonidc@singida.go.tz, ded@manyonidc.go.tz
Haki Ya Kunakiri ©2019 Halmashauri Ya Wilaya Ya Manyoni . Haki Zote Zimehifadhiwa.