- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
MkurugenziMtendaji pamoja na Maafisa Elimu Msingi wakipitia vitabu vilivyokabidhiwa na ChuoKikuu cha Aga Khan.
Halmashauri ya wilaya ya Manyoni imepokea jumla ya vitabu 1550 na vifaa 205 vya michezo kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kuweza kujifunza kusoma na kujenga tabia ya kujisomea vitabu wakiwa na umri mdogo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo la makabidhiano lililofanyika katika shule ya msingi Solya, Meneja Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan, Lucy Rweyemamu amesema kuwa Chuo Kikuu cha Aga Khan -Taasisi ya Maendeleo ya Elimu, Afrika Mashariki imeanzisha mradi wa kujisomea katika shule za msingi, wenye lengo la kuinua uwezo wa wanafunzi kuweza kujua kusoma na kuongeza ari ya kupenda kujisomea kuanzia wakiwa na umri mdogo nchini.
Rweyemamu amesema kuwa Chuo hiki kilianzisha mradi wa vilabu vya kujisomea mwaka 2013 katika shule za mkoa wa Dar es salaam pekee. Aliongeza kuwa, mwaka 2017 walipanua uwigo wa mradi huu katika mkoa wa Dodoma na miaka iliyofuata katika mikoa ya Mtwara, Morogoro na Arusha. Jumla ya idadi za shule zilizonufaika na mradi huu katika mikoa hii mitano ni shule 61. Shule kumi za mkoa wa Singida zinafanya jumla ya shule kuwa 71.
Aliongeza kuwa vilabu vya kujisomea ni hiari na kwamba wametengeneza mfumo ambao hautaweza kuingiliana na vipindi vya darasani.
“Kutokana na hilo tumeona ni vyema kupanua wigo zaidi na kuendeleza utekelezaji wa mradi huu katika mikoa mingine ambapo ni Iringa na Manyara na kuongeza shule 20 za ziada na kufikia shule 91 nchini. Leo hapa mkoani Singida wilaya ya Manyoni tutafanya jaribio la vitendo ambalo litawawezesha walimu, wanafunzi na wazazi kuweza kuelewa zaidi juu ya taratibu za uendeshaji wa klabu hizi.” Alisema Rweyemamu.
Aidha katika mkoa wa Singida ni wilaya mbili zinazonufaika na mradi huu kwa mara ya kwanza. Wilaya hizi ni Manyoni na Singida manisipaa na kwamba kila wilaya imepangiwa shule tano.
“Niongeze kuwa katika kufanikisha mradi huu, Chuo Kikuu cha Aga Khan kimetoa vitabu vya hadithi na vifaa vya michezo pamoja na mafunzo kwa walimu, wanafunzi na wazazi katika shule zilizoteuliwa juu ya uendeshaji wa klabu hizi. Chuo kitaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na ofisi ya Afisa Elimu ili kuendelea kutekeleza mradi huu.” Alifafanua Rweyemamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Melkzedeki Humbe ametoa shukrani kwa Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kuweza kugawa vitabu hivyo na vifaa hivyo vya michezo kwa shule za msingi Manyoni na ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuiona wilaya ya Manyoni kuwa ya kwanza katika kuzindua mradi huu.
“Nitoe rai kwa walimu katika shule zitakazokabidhiwa vitabu hivi kuimarisha hizo klabu za kujisomea kwa watoto na kuwahamasisha wanafunzi kuwa na ari ya kupenda kusoma vitabu. Alisisitiza pia walimu wazingatie kuhakikisha klabu hizi haziingiliani na kuitilafiana na vipindi vya madarasani.” Alisema Humbe.
Naye Afisa Elimu shule za msingi wilaya ya Manyoni Hamisi Milowe amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aga Khan katika kukuza viwango vya wanafunzi ili kuweza kundokana kabisa na tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika hivyo amewaagiza walimu kutunza vitabu hivyo na kutunza vifaa vya michezo.
Baadhi ya wazazi walioshiriki katika ufunguzi huo wametoa shukrani zao kwa Chuo Kikuu cha Aga Khan na kusema kuwa sasa wanaamini kuwa watoto wao wataweza kusoma na kuandika.
Shule ziolizokabidhiwa vitabu na vifaa vya michezo katika Halmshauri ya Wilaya ya Manyoni ni shule za msingi Solya; Muhalala;Tambukareli; Sayuni na Mwembeni.
HALMASHAURI YA WILAYA MANYONI
Sanduku la Posta: S.L.P 60 MANYONI
Simu: +255 26 2540136
Namba ya Simu: +255 26 2540136
Barua Pepe za Watumishi: ded.manyonidc@singida.go.tz, ded@manyonidc.go.tz
Haki Ya Kunakiri ©2019 Halmashauri Ya Wilaya Ya Manyoni . Haki Zote Zimehifadhiwa.