- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma Zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mh. Rahabu Mwagisa Solomon amezindua kampeni ya Upandaji miti katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni leo Tar 19.12.2018, zoezi ambalo limefanyika katika eneo la Stand kuu ya mabasi ya mji wa Manyoni.
Mkuu wa wilaya aliambatana na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Ndg. Charles E. Fussi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Manyoni Ndg. Charles Mkama pamoja na Viongozi mbalimbali wa Vijiji, Kata na Wilaya ambapo wote walishiriki katika zoezi na zaidi ya miti 100 imepandwa katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Manyoni Mh. Rahabu Mwagisa Solomon amewasisitiza viongozi wa vijiji na vitongoji kusimamia upandaji na utunzaji wa miti kila kaya na liwe endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadaye. Katika kuhimiza utunzaji wa miti na mazingira, Mkuu wa Wilaya ameonya utupaji wa taka ovyo pamoja na ukataji wa miti ovyo ambao umekuwa ukiharibu mazingira, na amewaonya wanaofyeka maeneo bila kufuata utaratibu kuacha mara moja.
Akizungumza kuhusiana na masuala ya kilimo Mh. Rahabu amewaomba wakulima katika kipindi hiki cha mvua kulima mbegu bora hasa kwa kufuata ushauri wa kitalamu kutoka kwa maafisa wa kilimo wa wilaya na amewahimiza wataalamu wa kilimo kutembelea kwa wananchi ili kujua changamoto zao na kuwashauri namna bora na sahihi ya mambo ya kilimo.
Mkuu wa wilaya pia ameisisitiza jamii kujitokeza kushiriki katika shughuli za kijamii hasa katika suala la elimu ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaenda shule ifikapo januari, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya elimu katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni zaidi ya wanafunzi 2300 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka 2019.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni Ndg. Charles E. Fussi ametoa wito kwa wananchi katika kupanda miti maeneo wanayoishi ili kuboresha mazingira, vilevile kutii sheria za nchi na kuonyesha ushirikiano kwa watendaji wa idara zote za halmashauri hasa kwa kushiriki katika mambo ya maendeleo pamoja na huduma za jamii. Amesisitiza kuwa iwapo kuna matukio ambayo wanaona yanawakosesha amani ikiwemo kuonewa au kunyimwa haki hasa sehemu za huduma za kijamii ikiwemo huduma ya afya, watoe taarifa ama wafike ofisini kwake, yuko tayari kupokea malalamiko ili kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati sahihi.
HALMASHAURI YA WILAYA MANYONI
Sanduku la Posta: S.L.P 60 MANYONI
Simu: +255 26 2540136
Namba ya Simu: +255 26 2540136
Barua Pepe za Watumishi: ded.manyonidc@singida.go.tz, ded@manyonidc.go.tz
Haki Ya Kunakiri ©2019 Halmashauri Ya Wilaya Ya Manyoni . Haki Zote Zimehifadhiwa.